Tanzania yaandaa
mkutano wa Magavana
Na Eleuteri Mangi-
MAELEZO
Tanzania inatarajia
kuwa mwenyeji wa Mkutano wa 30 wa mwaka wa Bodi ya Magavana wa Benki (BOG) utakaofanyikia
jijini Dar es salaam tarehe 22 mwezi huu.
Kwa mujibu wa taarifa
ya pamoja iliyotolewa jana jijini Dar es salaam na Katibu Mkuu Wizara ya Fedha
Dkt. Servacius Likwelile na Rais wa Benki ya PTA kwa vyombo vya habari, mkutano
huo utakuwa wa siku moja.
Taarifa hiyo imeeleza
kuwa lengo la mkutano huo ni kujadili
masuala mbalimbali ya kibenki ikiwemo mpango mkakati wa benki hizo na masuala
ya fedha na uchumi kwa nchi washirika.
Wajumbe wa mkutano huo
ni Mawaziri wa Fedha na uchumi wa nchi washirika ambao ndio chombo cha juu cha
ngazi ya maamuzi ya benki katika nchi zao.
Aidha, taarifa hiyo
imeongeza kuwa mkutano huo utatanguliwa
na semina ya wafanyabiashara itakayofanyika Agosti 21 siku moja kabla ya
mkutano mkuu wa Magavana hao.
Benki ya PTA
ilianzishwa mwaka 1985 ikiwa na jumla ya washirika 22 ikiwemo nchi 18 ambazo ni
Burundi, Comoros, Djibouti na Congo.
Nchi nyinine ni Misri, Eritrea,
Ethiopia, Kenya, Malawi, Mauritius, Rwanda, Seychelles, Somalia, Sudan, Uganda,
Zambia, Zimbabwe na mwenyeji Tanzania.
Aidha, PTA
inashirikiana na nchi nyingine nje ya bara la Afrika ambazo ni Belarus na China.
Washirika wengine Benki
ya Maendeleo ya Afrika (ADB), Kampuni ya Bima ya Mauritia iitwayo Eagle na
Mfuko wa Hifadhi ya Jamii wa Mauritius.