Kamati ya Kudumu ya Ardhi maliasili na Utaliileo imetembelea MRADI wa Samia Housing uliopo Kawe jijini Dar es Salaam ambao kwa sasa umefikia asilimia 65 ambapo ukikamilika utagharimu Bilioni 466.
Shirika linaendelea na Mpango wa ujenzi wa nyumba 5,000 za gharama ya kati chini kupitia mradi wa Samia Housing Scheme (SHS) ambao utekelezaji wake unaendelea. Mradi huu wa nyumba za kuuza na kupangisha unakusudia kuenzi kazi nzuri anazofanya Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ikiwemo kuwezesha upatikanaji wa nyumba bora nchini.
Asilimia 50 ya nyumba hizi zitajengwa katika Mkoa wa Dar es Salaam, asilimia 20 katika mkoa wa Dodoma na asilimia 30 zitajengwa katika mikoa mingine. Mradi huu utakaokuwa na nyumba 5,000 unaotekelezwa kwa awamu, utagharimu takriban Shilingi bilioni 466 sawa na Dola za Kimarekani milioni 200. Katika kuendeleza mradi huu, maandalizi ya ujenzi wa Mradi wa Samia Housing Scheme wenye nyumba 100 Jijini Dodoma na nyumba 560 eneo la Kawe awamu ya pili yanaendelea kukamilishwa.
Nyumba 560 zinaendelea kujengwa katika eneo hili la Kawe, Dar es Salaam ambapo hadi kufikia tarehe Juni 30, 2024, ujenzi umefikia asilimia 65. Mradi huu wa Kawe utagharimu shilingi bilioni 48.27 na hadi sasa shilingi bilioni 21.88 zimeshatumika. Mauzo ya mradi huu yamefikia asilimia 100 na Shirika limeshapokea malipo ya awali ya kiasi cha shilingi bilioni 31.2 na kiasi kilichobakia cha shilingi bilioni 45.5 kinaendelea kukusanywa.



