Kutokana na takwimu zilizotolewa na Wakala wa Usajili Ufilisi na Udhamini (RITA), za ongezeko la vifo na wimbi la talaka katika jamii, Waziri wa Katiba na Sheria Balozi Dkt. Pindi Chana amesema amepanga kukutana na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, George Simbachawene na Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu kutafuta suluhisho ya tatizo hilo.
Balozi Dkt. Chana amesema takwimu zinaonesha kumekuwa na ongezeko la vifo kwa wanaume vinavyosababishwa na magonjwa ya kuambukiza na yasiyoambukiza jambo ambalo linasababisha ongezeko la watoto waishio kwenye mazingira yasiyo bora pamoja na kukosa malezi ya pande zote mbili.
Aidha Waziri Chana amesema kuwa kwa upande wa hali ya ndoa, takwimu zinaonesha ongezeko la usajili wa talaka limekuwa kubwa kwa kila mwaka jambo linalochangia kwa kiasi kikubwa ukatili kwa watoto kwa kukosa malezi ya wazazi wawili.
Akizindua taarifa ya takwimu ya matukio muhimu ya binadamu pamoja na kufungua mafunzo ya uendelevu wa usajili wa watoto ya Wakala wa Usajili Ufilisi na Udhamini (RITA) Jijini Dodoma Waziri Dkt. Pindi Chana amesema katika takwimu za sensa kuhusu hali ya ndoa kwa mwaka huu RITA wamesajili talaka 800 ikilinganishwa na miaka ya nyuma ambayo ilikuwa ni chini ya hapo hivyo ni wajibu wa Serikali kukaa na kuona wananusuru hali hii.
“Nahitaji kikao na Waziri wa Mambo ya Ndani ili tukae tuzungumze, takwimu za ajali, vifo kama tulivyoambiwa na taarifa ya RITA, tunafanyaje, haraka sana nahitaji kikao na waziri mwenzangu dada yangu Ummy Mwalimu, lazima tushirikishe hizi data ili tupate kujua tunafanyaje” Amesema Waziri Pindi Chana.
Uzinduzi wa taarifa ya matukio muhimu ya binadamu na ufunguzi wa mfumo endelevu wa usajili wa watoto na kikao kazi kuhusu uendelevu wa usajili wa watoto katika vituo tiba na ofisi za kata umehusisha maofisa usajili kutoka mikoa mbalimbali nchini, wadau wa maendeleo pamoja na maofisa waandamizi kutoka wizara na taasisi za Serikali.
.jpeg)