WAZIRI SIMBACHAWENE AMPONGEZA MHE. RAIS KWA KUTEKELEZA MIRADI YA MAENDELEO INAYOWAGUSA WANANCHI WOTE

 

Waziri wa Nchi, Ofisi ya  Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. George Simbachawene na Mbunge wa Jimbo la Kibakwe   amempongeza Rais Mhe. Samia Suluhu Hassan katika kipindi chake cha uongozi kwa kujipambanua kutoa fedha nyingi kwa ajili ya kutekeleza miradi ya  maendeleo inayowagusa wananchi wa chini moja kwa moja 


 Ametoa kauli hiyo leo wakati Mwenge wa Uhuru ukiwa   katika Kijiji cha Itende Kata ya Pwaga  wilayani Mpwapwa Mkoani Dodoma ambapo umekagua na kuweka jiwe la msingi katika  Mradi wa Maji wenye thamani ya Shilingi Bilioni 4 utakaohudumia vijiji vitatu pamoja na vitongoji vitatu


Akizungumzia utekelezaji wa Mradi huo wa maji, Mhe. Simbachawene amesema shabaha ya  Rais Mhe. Samia Suluhu Hassan ni kuona huduma za msingi ikiwemo maji yanapatikana kwa urahisi bila kulazimika wananchi kusafiri umbali mrefu kuifuata huduma hiyo


Katika hatua nyingine  Mwenge wa Uhuru ukiwa  katika Kata ya Rudi wilayani humo   umekagua utekelezaji wa shughuli mbalimbali ikiwemo uwekaji wa  jiwe la msingi kwenye  jengo la maabara  lililotekelezwa kwa thamani ya  Sh. Milioni 94.


Awali, akizungumza Kiongozi wa Mbio za  Mwenge Kitaifa, Bw. Godfrey Mzava ameridhishwa na  utekelezaji wa mradi wa maji huku akisema taratibu  zote za manunuzi zilifuatwa wakati wa utekelezaji wa mradi huo.


Bw.Mnzava amesema Mhe.Rais amedhamiria kuhakikisha huduma za kijamii ikiwemo maji umeme ziapatikana kwa wananchi wote bila kujali mahali walipo 


Ameongeza kuwa Agenda kuu ya Mbio za Mwenge mwaka huu ni kutunza mazingira na kuhamasisha ushiriki wa uchaguzi wa mitaa


Kwa mujibu wa  taarifa Mwenge wa Uhuru Mkoani Dodoma  unapita kukagua idadi ya miradi 56 yenye thamani ya Sh.Bilioni 21.2 ambapo utakimbizwa kwa siku nane katika wilaya saba Mkoa huo kwa umbali wa kilomita 1484


Mwenge wa Uhuru kwa mwaka huu  unaongoza na kauli mbiu ya ‘’Tunza Mazingira na Shiriki Uchaguzi wa Serikali za Mitaa kwa Ujenzi wa Taifa endelevu’’








 

MWISHO

Post a Comment

Previous Post Next Post