JESHI LA ZIMAMOTO NA UOKOAJI LAADHIMISHA SIKU YA WAZIMAMOTO DUNIANI,WAMSHUKURU RAIS SAMIA






JESHI la Zimamoto na Uokoaji Tanzania Bara linaungana na Wazimamoto wote Duniani kuadhimisha Siku ya Wazimamoto Duniani ambayo hufanyika Mei 4 ya kila Mwaka.

Akizungumza na waandishi wa habari leo Mei 4, 2025 jijini Dar es Salaam Naibu Kamishana wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji na Msemaji wa Jeshi hilo Puyo Nzalayamisi amesema maadhimisho haya yanatambua mchango mkubwa wa Maafisa na Askari wa Zimamoto na Uokoaji katika kulinda maisha na mali za wananchi dhidi ya majanga mbalimbali ikiwemo moto, matetemeko ya ardhi, mafuriko, maporomoko ya ardhi, ajali za barabarani na majanga mengine.

"Siku hii ilianzishwa rasmi mwaka 1999 kufuatia tukio la kusikitisha lililotokea nchini Australia, ambapo Wazimamoto watano walipoteza maisha wakijaribu kuzima moto mkubwa wa msitu katika eneo la Linton, Jimbo la Victoria. Tukio hilo liliamsha mshikamano na hisia za heshima kwa mashujaa wa zimamoto duniani kote na kupelekea kuanzishwa kwa siku maalumum ya wafanyakazi," amesema Naibu Kamishna Nzalayamisi.

Naibu Kamishna Nzalayamisi amesema malengo ya maadhimisho hayo ni kutoa heshima kwa Wazimamoto waliopoteza maisha wakiwa kazini, kutambua mchango wa Wazimamoto waliopo hai katika jamii na kuelimisha umma kuhusu majukumu ya Jeshi la Zimamoto na hatua za tahadhari.

Malengo mengine ni kujenga mshikamano wa kimataifa kati ya vyombo vya Zimamoto na Uokoaji na kutoa motisha kwa Zimamoto kuendelea kutekeleza majukumu yao kwa moyo wa uzalendo.

Kwamba kwa mwaka huu, Jeshi la Zimamoto na Uokoaji limefanya shughuli mbalimba za kijamii ikiwa ni sehemu ya maadhimisho hayo ambapo ametaja shughuli hizo kuwa ni pamoja na kufanya usafi wa mazingira katika Hospitali ya Mkoa wa Njombe na Kituo cha Sfya Msamala-Ruvuma na utoaji wa msaada wa kibinadamu katika Gereza la Mkoa wa Lindi.

Shughuli nyingine ni utoaji wa elimu kwa umma kuhusu kinga na tahadhari dhidi ya moto katika shule, masoko, vituo vya mabasi, mikusanyiko ya watu na kupitia vyombo vya habari, uchangiaji wa damu kwa hiari kwa ajili ya wahitaji na kupandishwa vyeo kwa baadhi ya Maafisa na Askari waliotimiza wajibu wao kwa weledi na kujitolea.

Ametumia fursa hiyo kumshukuru Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuliwezesha Jeshi hilo katika kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi ambapo pia ameeleza kuwa wanatambua mchango mkubwa wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, vyombo vingine vya ulinzi na usalama na wananchi wanaoshirikiana nao kwa kutoa taarifa kwa haraka pindi majanga yanapotokea.

Post a Comment

Previous Post Next Post