WAZIRI MKUU MAJALIWA MGENI RASMI SIKU YA NYUKI DUNIANI



Na Mwandishi Wetu - Dodoma

Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa (Mb) anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika kilele cha maadhimisho ya Siku ya Nyuki Duniani Kitaifa yatakayofanyika   katika viwanja vya Chinangali jijini Dodoma.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini humo, Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Balozi Dkt. Pindi Chana (Mb) alisema maadhimisho hayo ni uzingatiwaji wa  Azimio la Bazara Kuu la Umoja wa Mataifa na yamelenga kutambua umuhimu na mchango wa Nyuki katika maisha ya mwanadamu ambapo kilele chake hufanyika Mei 20 kila mwaka. 

“Sote tunatambua kuwa nyuki na wadudu wengine wachavushaji wanamchango mkubwa sana katika usalama wa chakula, pamoja na uhifadhi bioanuwai na asilimia 80 ya mazao yote ya chakula hutegemea kuchavushwa na mdudu nyuki” alisema Dkt. Chana.

Alisema kuwa pamoja na umuhimu wake bado mdudu nyuki yuko hatarini kutoweka kutokana na shughuli za binadamu na kuwa  maadhimisho ya mwaka huu yatasaidia kupeleka  ujumbe kwa watanzania na dunia kwa ujumla juu ya umuhimu wa kumlinda nyuki pamoja na kutunza mazingira yake.  

Maadhimisho ya mwaka huu yanabebwa na kauli mbiu ya ‘‘Nyuki kwa Uhai na Uchumi Imara, Tuwahifadhi’’ ambayo inaakisi maono na mwelekeo wa serikali ya awamu ya sita chini ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan.

Aidha, Mhe. Dkt. Chana alisema maadhimisho hayo yatafanyika sambamba na shughuli mbalimbali kwa siku nne ikiwemo maonesho ya wanyapori hai, pia yatajumuisha matamasha ya nyuki mtaa kwa mtaa.

Pia kutakuwa na semina muhimu itakayohusu mnyororo wa thamani katika ufugani wa nyuki utakaoongozwa na wataalam wabobezi kutoka wizarani na wadau wa nje.

Mhe. Dkt. Chana aliongeza kuwa kutakuwa na ziara ya mafunzo kwa wadau ambao watakwenda kwenye viwanda vinavyojihusisha na mazao yatokanayo  na nyuki.

Alisema wakati wote wa maonesho Tiba Nyuki itatolewa bure kwa wananchi watakaotembelea na kuhitaji huduma hii ambayo inasaidia kuimarisha kinga ya mwili. 

“Katika eneo la maonesho kutakuwa na vivutio mbalimbali vya kitalii wakiwemo Wanyamapori hai kama Simba, Tembo, Ndege Tausi na wanyama wengine” alisema Mhe. Dkt. Chana.

Aidha Waziri Chana ametoa rai kwa watanzania wote hususan wakazi wa Jiji la Dodoma na mikoa ya jirani kuungana na Wizara hiyo katika kuadhimisha tukio hilo muhimu na adhimu kwa wananchi na taifa kwa ujumla.

Post a Comment

Previous Post Next Post