Leo asubuhi, Mbunge wa Jimbo la Kibamba, Mheshimiwa Angellah Jasmine Mbelwa Kairuki, amekabidhi viti mwendo (wheelchairs) 10 kwa watu wenye mahitaji maalum, hatua inayolenga kuwawezesha kufanya shughuli zao za kila siku kwa urahisi zaidi.
Msaada huo umepokelewa kwa furaha kubwa na walengwa pamoja na familia zao, wakieleza kuwa viti hivyo vitawarahisishia usafiri na kuboresha maisha yao kwa ujumla.
Miongoni mwa waliopatiwa msaada ni Jackson, ambaye licha ya ulemavu wa kutotembea, ameonesha bidii kwa kuanzisha genge duka pamoja na huduma ya uwakala wa kifedha. Kutokana na juhudi zake, Mheshimiwa Kairuki ameongeza mtaji wa biashara yake kwa kumpatia shilingi laki tano (500,000).
Wazazi na walezi wa walionufaika wamemshukuru Mbunge Kairuki kwa moyo wake wa kujali na kwa kuendelea kugusa maisha ya watu wenye mahitaji maalum.
Akizungumza katika tukio hilo, Mheshimiwa Kairuki amesema ataendelea kutoa msaada wa viti mwendo kwa utaratibu maalum, akizingatia kuwa mahitaji ni makubwa.






