STARS YAREJEA DAR, KAZIMOTO NDANI
Kikosi cha Taifa Stars kimerejea jijini Dar es Salaam
leo kutoka Mbeya ambapo Jumapili (Julai 20 mwaka huu) kitapambana na Msumbiji
(Mambas) kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Benchi la Ufundi la Taifa Stars pamoja na wachezaji
kesho (Julai 19 mwaka huu) saa 5 asubuhi watakuwa na mkutano na waandishi wa
habari kwenye hoteli ya Protea Courtyard iliyopo Upanga Seaview jijini Dar es Salaam.
Naye mchezaji Mwinyi Kazimoto amewasili leo 1.30 asubuhi
kwa ndege ya Qatar Airways kutoka Qatar ambapo anacheza mpira wa miguu katika
klabu ya Al Markhiya ya huko. Stars inayodhaminiwa na Kilimanjaro Premium Lager
imepiga kambi katika hoteli ya Protea Courtyard.
SERENGETI BOYS MORALI JUU
Kocha Mkuu wa Serengeti Boys, Hababuu Ali Omari amesema
morali ya wachezaji wake ipo juu kwa ajili ya mechi dhidi ya Afrika Kusini
(Amajimbos) itakayochezwa kesho (Julai 18 mwaka huu).
Mechi hiyo ya kwanza ya raundi ya pili ya michuano ya
Afrika kwa vijana wenye umri chini ya miaka 17 itafanyika kwenye Uwanja wa Azam
Complex uliopo Chamazi jijini Dar es Salaam kuanzia saa 10 jioni.
Akizungumza kwenye mkutano na waandishi wa habari kwenye
ofisi za TFF jijini Dar es Salaam leo, Kocha Hababuu amesema nia ya kikosi
chake ni kuhakikisha wanafika kwenye fainali za Afrika zitakazofanyika mwakani
nchini Niger.
“Tunaiheshimu Afrika Kusini, lakini hatuiogopi. Morali
ya wachezaji ipo juu na wanajiamini. Kimsingi wanajua kuwa hii ndiyo njia ya
wao kutokea kwenye mpira wa miguu, kwa hiyo lengo ni kushinda,” amesema Kocha
Hababuu.
Naye Kocha wa Afrika Kusini, Molefi Ntseki amesema anaziheshimu
timu za Tanzania, na changamoto aliyonayo ni kuhakikisha kuwa anashinda mechi
hiyo kwani mara ya mwisho kwa timu yake kushiriki fainali za Afrika ilikuwa
miaka sita iliyopita.
Kiingilio katika mechi hiyo ni sh. 2,000 na tiketi
zitapatikana uwanjani kwenye magari maalumu.
MSUMBIJI KUTUA MCHANA DAR
Timu ya Taifa ya Msumbiji (Mambas) inawasili Dar es
Salaam kesho (Julai 18 mwaka huu) kwa ajili ya mechi ya michuano ya Afrika
dhidi ya Taifa Stars itakayochezwa Jumapili, Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Mambas itatua Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius
Nyerere (JNIA) saa 7.30 mchana kwa ndege ya LAM ikiwa na msafara wa watu 37
ambapo kati ya hao, 25 ni wachezaji.
Wachezaji kwenye msafara huo ni Almiro Lobo, Apson
Manjate, Bone Mario Uaferro, Dario Ivan Khan, Edson Sitoe, Eduardo Jumisse, Gelicio
Aurelio Banze, Helder Pelembe, Josemar Machaisse, Elias Pelembe, Isac Carvalho
na Jeffrey Constatino.
Wengine ni Manuel Fernandes, Manuel Uetimane, Mario
Sinamunda, Momed Hagi, Reginaldo Fait, Reinoldo Mandava, Ricardo Campos, Saddan
Guambe, Simao Mate Junior, Soares Victor Soares, Stelio Ernesto, Vando Justino
na Zainadine Junior.
Timu hiyo itafikia kwenye hoteli ya Accomondia, na
itaondoka Jumapili mara baada ya kumalizika kwa mechi hiyo itakayochezeshwa na
mwamuzi Mahmoud Ashour.
LINA KESSY AUTEULIWA KUWA OFISA MICHEZO AU
Mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya Shirikisho la Mpira wa
Miguu Tanzania (TFF), Lina Kessy ameteuliwa kuwa Ofisa Michezo wa Umoja wa
Afrika (AU).
Uteuzi huo umefanywa na Mwenyekiti wa Kamisheni ya AU,
Nkozasana Dlamini-Zuma, na Lina atatumikia nafasi hiyo kwa mkataba wa miaka
mitatu katika makao makuu ya AU yaliyopo Addis Ababa, Ethiopia.
Lina ambaye pia ni Mwenyekiti wa Chama cha Mpira wa
Miguu wa Wanawake Tanzania (TWFA) amewashukuru wote ambao kwa michango yao ya
hali na mali imemwezesha kufika hapo.
Ameishukuru TFF kwa kumlea na kumjenga. Shukrani
nyingine amezitoa kwa Serikali kupitia Kurugenzi ya Michezo, Baraza la Michezo
la Taifa (BMT) na Kamati ya Olimpiki Tanzania (TOC).
TFF inampongeza kwa uteuzi huo, na tunaamini
ataipeperusha vyema bendera ya Tanzania ikiwemo kuwa chachu ya maendeleo ya
michezo kwa Tanzania na Afrika kwa ujumla.
BONIFACE WAMBURA
OFISA HABARI NA MAWASILIANO
SHIRIKISHO LA MPIRA WA MIGUU TANZANIA (TFF)