Mathayo 5, 7 & 16, Yohana 17)
Somo hili limetafsiriwa
kutoka katika Copr. 2011, Bruce N. Cameron, J.D. Marejeo yote ya maandiko
yametoka kwenye tafsiri ya New International Version (NIV), copr. 1973, 1978,
1984 International Bible Society, isipokuwa kama itaelezwa vinginevyo. Nukuu
kutoka kwenye tafsiri ya Biblia ya NIV inatumika kwa ruhusa ya Wachapishaji wa
Biblia wa Zondervan. Majibu yaliyopendekezwa yanapatikana kwenye parandesi
(kwenye mabano). Somo limekaa kimtazamo kwamba mwalimu anatumia ubao au sehemu
nyingine yoyote ambayo inaweza kuonekana na wanafunzi. Kama huwa una kawaida ya
kupokea somo hili kwa njia ya barua pepe na hukulipata kwa juma moja, unaweza
kulipata kwa kubofya kwenye www.lesoni.blogspot.com kwa lugha ya Kiswahili na
http://www.GoBible.org
kwa lugha ya Kiingereza pamoja na lugha nyingine kama vile Kifaransa,
Kijerumani. Omba kwa ajili ya uongozi wa Roho Mtakatifu unapojifunza.
Utangulizi: Sehemu kubwa ya kazi yangu kwa miaka mingi
imejihusisha na kushughulikia kesi zinazohusu uhuru wa dini. Huwa
ninawawakilisha “watu wadogo” pekee nikimanisha waajiriwa, katika nyanja za
uhuru wa dini mahala pa kazi. Hata hivyo, swali la msingi sana katika kesi ya
aina hii ni endapo mwajiriwa ana imani ya dhati katika dini. Nimejifunza
kuepuka kuwawakilisha waajiriwa wasio na mafungamano ya dhati na kanisa
mahalia. Watu ambao mara kwa mara wanaabudu katika kundi la waumini wana nafasi
kubwa ya kuwa na imani za dhati katika dini. Kwa nini hivyo? Hebu tujifunze
Biblia inachofundisha kuhusu muumini na kanisa!
I.
Mwamba
A.
Soma Mathayo 16:13. Unadhani kwa nini Yesu aliwauliza
wanafunzi wake swali hili?
B.
Soma Mathayo 16:14. Unafikiria nini kuhusu majibu haya?
(Hii ni orodha ya kufurahisha kuhusu uwezekano wa kwamba Yesu ni nani. Hata
hivyo, kwa hakika majibu haya sio sahihi.)
C.
Soma Mathayo 16:15-17. Petro analo jibu sahihi! Nani
aliyempa msukumo wa jibu hilo? (Mungu.)
D.
Soma Mathayo 16:18. Je, palikuwepo na utatanishi kuhusu
jina la Petro? Kwa nini Yesu anamwambia Petro, “Nami nakuambia, Wewe ndiwe
Petro?” (Kiyunani ni cha msingi hapa. Kwa Kiyunani Petro maana yake ni mwamba
mdogo, au kipande cha mwamba. Yesu anacheza na maneno, “Nakuambia ewe kipande
cha mwamba kwamba nitalijenga kanisa langu juu ya mwamba mkubwa.”)
1.
Unadhani nini maana ya jambo hilo? (Soma kile
anachokisema Petro kuhusu jambo hili katika 1 Petro 2:4-6. Petro anasema kwamba
Wakristo ni “mawe yaliyo hai” yanayojengwa kwenye “nyumba ya Roho.” Yesu ndiye
jiwe kuu la pembeni la nyumba hiyo.)
2.
Hebu turejee kwenye mwamba mkubwa katika Mathayo 16:18.
Unapotafakari mazungumzo ya wanafunzi na Yesu, unadhani “mwamba” (mwamba
mkubwa) unawakilisha nini? (Nadhani mwamba ambao Kanisa linajengwa juu yake ni kauli
ya Petro kwamba Yesu ni “Kristo, Mwana wa Mungu aliye hai.” Yesu ndiye jiwe kuu
la pembeni na uungu wake ni imani kuu.)
3.
Hebu turejee nyuma kidogo. Unadhani maana kamili ya
Mathayo 16:18 ni ipi? (Kwamba Kanisa linajengwa juu ya “mwamba” wa ufahamu kwamba Yesu ni Mungu, na Kanisa linajumuisha miamba
midogo midogo inayofahamu jambo hili, miamba kama vile Petro na wewe na mimi,
na milango ya kuzimu haitatushinda.)
E.
Soma Mathayo 16:19. Nani anayepewa “funguo” hapa?
(Inaonekana kama vile ni Kanisa – au angalao washiriki wa Kanisa. Inaweza iwe
vigumu sana funguo hizo kumaanisaha kuwa ni Yesu kwa kuwa Yesu hawezi kujipatia
funguo yeye mwenyewe.)
1.
Hii ni kauli madhubuti sana. Unadhani Yesu anamaanisha
nini anaposema kuwa Kanisa linapewa “funguo za ufalme wa mbinbguni,” au angalao
washiriki wa Kanisa wanatenda kazi pamoja kama Kanisa? (Nina uhakika sielewi
kikamilifu muktadha wa kauli hii, lakini angalao kauli hiyo inasema kuwa Kanisa
hufunua njia ya kwenda mbinguni. Kuwa katika kundi la waumini hutusaidia kuielewa
neema na mwenendo wa Kikristo.)
F.
Soma Mathayo 16:20. Ikiwa ukweli kwamba Yesu ni Mungu
ni mwamba ambao Kanisa linajengwa juu yake, kwa nini jambo hilo liwe siri?
(Mungu ana muda wake kwa ajili ya kila jambo. Huu ndio ukweli tunaopaswa kuwa
nao mawazoni mwetu tunapokatishwa tamaa na kutokutenda kwa watu wengine.)
II.
Mtazamo
A.
Soma Yohana 17:20-23. Tuna dhana nyingi sana zilizopo
kwenye haya mafungu. Kuna sababu gani ya kuwa na mtazamo wa umoja miongoni mwa
waumini? (“Ili ulimwengu upate kusadiki ya kwamba wewe ndiwe uliyenituma.”
Umoja ndani ya kanisa hutoa ujumbe chanya kwa walimwengu wasioamini.)
1.
Kiini cha ujumbe ni kipi? (Umoja hutokana na upendo.
Mungu anatupenda nasi tunapendana.)
2.
Je, kanisa lina hali gani katika kipengele hiki?
(Unaweza kuwa umegundua kwamba tulipokuwa tukijadili Mathayo 16:19 niliruka
lugha inayohusu Kanisa kufunga na kufungua masuala mbinguni na duniani. Ni
vigumu sana kwangu kuelewa jinsi jambo hili linavyohusika sasa hivi wakati kuna
makanisa mengi sana tena yenye viwango tofauti.)
3.
Kauli nyingine ya kupendeza katika Yohana 17:22 ni
kwamba Yesu “[ametupatia] utukufu ambao [Mungu Baba alimpa Yesu].” Je, huu
utukufu wa Kiungu ambao wewe na mimi tunao ni upi? (Nadhani ni utukufu wa
kushirikishwa na Mungu. Je, una ushirika fulani maishani unaokufanya upendeze?
Hivi sasa nina gari jipya ambalo watu huwa wananisimamisha na kulizungumzia.
Ikiwa una mwenzi mwenye mafanikio, watoto wenye mafanikio, kampuni yenye
mafanikio, mashirikiano yote haya yanakupatia “utukufu.” Kuwa mshirika wa karibu
wa Muumba wa Ulimwengu hutupatia utukufu.)
III.
Umoja Unapopata Pancha
A.
Soma Mathayo 7:1-2. Hili linaonekana kama jambo la
kujifunza kivitendo. Kuna tatizo gani katika kuwahukumu watu wengine? (Nawe
unahukumiwa kwa kiwango hicho hicho unachokitumia.)
1.
Je, tunazungumzia hukumu ya mwisho? Je, hukumu hiyo ina
kipimo kikubwa? Je, wale wasiojali chochote wanapata kiwango cha chini kabisa?
(Kwa mara nyingine, hili linaonekana kama jambo la kujifunza kivitendo, badala
ya kauli inayohusu hukumu ya mwisho.)
B.
Soma Mathayo 7:3-4. Unadhani kwa nini mifano yote
miwili, kibanzi na boriti, vinatengenezwa kwa mbao? (Nadhani huwa tunajielekeza
kuangalia dhambi zetu ndani ya watu wengine. Ni dhambi ile ile, isipokuwa tu
mtu mwingine anayo dhambi hiyo. Kimsingi, fungu linaashiria kwamba mtu
anayehukumu ana tatizo kubwa zaidi.)
C.
Soma Mathayo 7:5. Je, tunapaswa kuwa kwenye kazi ya
kuondoa boriti? Jambo hili linalenga kujua kama tumejiandaa kikamilifu?
1.
Je, ungependelea kuwa na kibanzi jichoni mwako?
(Maatizo ya dhambi maishani mwetu yanatukera. Yanatufanya tusiwe na raha. Mtu
mwenye tatizo hilo hilo anapoanza kutukosoa, tunakasirika – ingawa tungekuwa
bora zaidi pasipo uwepo wa tatizo la dhambi.)
a.
Mara zote nimekuwa nikidhani kwamba mtu mwenye uzoefu
na dhambi fulani yuko kwenye nafasi nzuri zaidi kuwashauri watu wengine kuhusu
dhambi hiyo. Je, hiyo ni kweli? (Nadhani hiki ndicho kinachomaanishwa na kauli
ya “ndipo utakapoona vema kukitoa kile kibanzi.” Ikiwa, kwa uwezo wa Roho
Mtakatifu, umeshinda tatizo kubwa la dhambi, unaweza kuona suluhisho “kwa wazi
zaidi.”)
2.
Je, mambo yote haya yanahusianaje na umoja? (Kuwakosoa
watu wengine juu ya dhambi zile zile maishani mwako husababisha
ugomvi/migongano na mgawanyiko. Kumsaidia mtu ili ashinde dhambi uliyoishinda
huleta mbaraka.)
a.
Je, hiyo inapaswa kuwa kanuni kanisani – wale tu
waliotaabika na kupambana na dhambi ndio wanaoweza kutoa maoni kwenye dhambi
hiyo kwa watu wengine?
D.
Soma Mathayo 7:6. Je, Yesu amebadili mada?
1.
Ikiwa tupo kwenye mada hiyo hiyo, je, lulu za dhati ni
zipi? (Ushauri wako uliojengwa kwenye uzoefu wako mwenyewe. Mjadala wako kuhusu
jinsi ulivyotawaliwa na dhambi katika eneo hilo. Mbwa na nguruwe hawatanufaika
na ufunuo wako wa dhati wa matatizo ya zamani, matatizo hayo “yatakugeuza na
kukuvunja vipandevipande.”)
IV.
Kuziba Pancha
A.
Soma Mathayo 5:23-24. Je, watu hawa wanafanya nini mara
wanapokumbuka kutokuelewana na mtu fulani? (Wapo madhabahuni – ikimaanisha
kwamba wana mwenendo mzuri na Mungu. Mara kwa mara, kuenenda vizuri na Mungu
huhusisha dhambi inayoleta athari chanya kwa watu wengine. Katika hali ya
kawaida utakuwa ukimfikiria mtu huyu wakati ulipokuwa ukitubu dhambi yako kwa
Mungu.)
1.
Je, tunamzungumzia mtu ambaye amekukosea? (Hapana. “Ndugu
yako ana neno juu yako.”)
2.
Je, tunazungumzia halia ambayo wewe binafsi huna
makosa? (Fungu halizungumzii chochote juu ya nani mwenye makosa. Linasema tu
kwamba mtu fulani hana amani na wewe.)
3.
Je, tunatakiwa kuwafanyia nini watu wenye kinyongo
dhidi yetu? (Tunaendele na kutafuta suluhu.)
4.
Nimegundua Yesu anatumia neno “ndugu.” Je, hilo ni la
muhimu sana? (Soma Luka 6:22-23. Watu hawa wana jambo dhidi yako, na mara hii
huu ni mbaraka. Nadhani jambo hili linarejea kwenye mjadala wa mbwa na kondoo
uliopo katika Mathayo 7:6. Tatizo linapokuwa miongoni mwa washiriki unatakiwa
kulifanyia kati kulitatua. Tatizo linapoibuka kwa wapagani kwa sababu wewe ni
mwaminifu kwa Mungu, basi haiwezekani kujaribu kutafuta sukuhu. Nguruwe wa
kipagani watakugeukia na kukuganyagia chini.)
B.
Rafiki, je, upo kanisani na kanisa lako lina umoja?
Kanisa ni chombo muhimu cha Mungu cha kuiendeleza injili. Endapo wewe au kanisa
lako mnapitia uzoefu wa gurudumu lenye pancha inapokuja kwenye suala la umoja,
je, utajitoa leo kujaribu kurejesha umoja?