Na Humphrey Shao, Globu ya Jamii
Tasisi isiyo ya kiserikali inayojishughulisha na tafiti katika masuala ya elimu nchini ya Haki elimu imemwaga sifa kwa serikali ya awamu ya tano kwa jisni ilivyoweza kuboresha sekta ya elimu kwa kipindi chake cha miaka mitatu iliyokaa madarakani tangu Rais Dk John Pombe Magufuli achaguliwe.
akizungumza na Waandishi wa habari jijini Dar es Salaam leo wakati wa mapitio ya bajeti ya Wizara ya elimu ya mwaka 2019/2020 Mkurugenzi wa Shirika la Haki Elimu Dk.John Kalaghe amesema kuwa Mwaka wa
Fedha 2018/2019 unakamilisha kipindi cha miaka mitatu ya serikali ya Awamu ya Tano chini ya Rais John Pombe Magufuli Miradi mikubwa ya maendeleo ya kiuchumi na
kijamii imeanzishwa na inaendelezwa katika awamu hii.
"Ukiitazama sekta ya elimu
ongezeko la udahili wa wanafunzi
katika ngazi zote za elimu ni mojawapo ya mafanikio makubwa yaliyochagizwa na
serikali ya Rais John Pombe Magufuli. Udahili
wa watoto katika shule za msingi
umeongezeka kwa 17% kutoka wanafunzi 8,639,202 mwaka 2016 hadi wanafunzi
10,111,255 mwaka 2018 (AJESR) 2018. Vivyo hivyo, kumekuwa na ongezeko la 12.6%
ya wanafunzi katika shule za sekondari kutoka wanafunzi 1,908,857 mwaka 2017 hadi
2,148,466 mwaka 2018"alisema Dk Kalage.
amesema Udahili katika shule za msingi umefikia karibu na kiwango
kilichowekwa kimataifa kwa asilimia
96.9% (kwa watoto wote walioandikishwa bila kuzingatia umri) na asilimia 84% (kwa
watoto walioandikishwa wakiwa na umri sahihi wa kuanza shule). Zaidi ya 70% ya
wanafunzi wote wanaomaliza darasa la saba wanaendelea na elimu ya sekondari.
Mafanikio haya tunayoyaona yamechangiwa na uamuzi wa Serikali ya Awamu ya Tano
wa kuondoa ada katika elimumsingi.
ametaja kuwa licha ya mafanikio haya Lakini mazuri, bado kuna changamoto kadhaa ambazo zinaikabili sekta
ya elimu. Changamoto hizi has ni zile
zinazosababishwa na upungufu wa fedha zinazotengwa na zinazopelekwa
katika sekta hii. Kwa mfano, wakati udahili wa wanafunzi umeongezeka kwa
wastani wa 17% kama ilivyoelezwa hapo juu, idadi ya shule imeongezezeka kwa 1% tu kwa shule zote za msingi na
sekondari tangia mwaka 2016. Ripoti ya Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG)
ya mwaka wa fedha 2016/17, inaonesha upungufu wa 85% ya madarasa kwa shule za
msingi, 83% kwa mashimo ya choo, 66% kwa nyumba za walimu na 14% kwa madawati. Aidha, shule za sekondari
zina upungufu wa 52% ya madarasa, 84% ya maabara, 86% ya madawati, 85% ya nyumba
za walimu na vilevile 88% ya mabweni na 53% ya mashimo ya choo. Jambo hili
linashtua sana.
amesema HakiElimu
tukiwa mojawapo ya wadau muhimu katika sekta ya elimu, tunalo jukumu la kuishauri serikali pamoja na
bunge na kupendekeza njia sahihi za kufikia malengo ya mipango ambayo serikali
imeweka ili kufanikisha elimu bora kwa wote. Wakati huu ambapo wabunge na wizara zinakaa kwa ajili ya kupanga
bajeti kwa mwaka wa fedha 2019/20, HakiElimu inatumia fursa hii kutoa mapendekezo
ya maeneo ambayo tunadhani ni muhimu
kuzingatiwa kama ifuatavyo:
Kuongeza bajeti ya sekta ya elimu: Katika vipindi vitatu vya miaka
ya fedha iliyopita, bajeti ya elimu imekuwa ikishuka kwa tabribani asilimia moja
kila mwaka. Mathalani mwaka 2016/17
bajeti ilikuwa Tsh bilioni 4,770 lakini
ikashuka hadi kufikia Tshs bilioni 4,706 katika mwaka wa fedha 2017/18 na mwaka
2018/19 bajeti iliyoidhinishwa ilishuka zaidi
hadi kufikia Tshs bilioni 4,628. Katika hali ya kawaida tungetegemea bajeti ya sekta ya elimu
ingepanda ili kukidhi mahitaji ya ongezeko la wanafunzi wanaodahiliwa na utekelezaji wa elimumsingi
bila ada. Kielelezo kifuatacho
kinaonesha mwenendo wa bajeti kwa miaka mitatu iliyopita mfululizo.
Uwiano
kati ya bajeti ya sekta ya elimu na bajeti kuu ya serikali umeshuka na kupungua
chini ya viwango vinavyokubalika kikanda na kimataifa, vikiwamo viwango
vilivyowekwa na Tamko la Incheon ( 2015) ambalo linazitaka nchi za kusini mwa Jangwa
la Sahara kutenga 20% ya bajeti ya serikali kwenda sekta ya elimu. Uwiano wa
bajeti ya elimu kwenye bajeti ya serikali (ukijumuisha deni la taifa) umepungua
kutoka 16.1% kwa mwaka 2016/17 hadi 15% kwa mwaka 2017/18 na kushuka zaidi hadi
kufikia 14% kwa mwaka 2018/19. Kwa kuzingatia ongezeko la bajeti ya taifa
katika miaka mitatu na kama serikali
ingetenga walau 20% kwa sekta ya elimu,
bajeti ya sekta ya hii ingeongezeka kwa jumla ya Tshs bilioni 4,666.
Kama kiwango
hiki kingepangwa na kutolewa kingepunguza kwa kiasi kikubwa changamoto za
miundombinu tulizozitaja awali.
HakiElimu
inaishauri serikali, wizara husika na wabunge kuchagiza ongezeko la bajeti na
uwiano wa bajeti ya sekta ya elimu na ule wa bajeti ya serikali kufikia 20%.
Waziri wa Nchi,
Ofisi ya Rais TAMISEMI, Selemeni Jafo, alitoa ahadi ya kupeleka kiasi cha Tsh 29
bilioni kwa ajili ya miundombinu katika shule za kidato cha tano na sita. Fedha
hizo zililenga kujenga madarasa 478 na mabweni 269 kwa ajili ya wanafunzi
21,808 waliokuwa wanatarajia kujiunga na kidato cha tano lakini hawakuweza
kufanya hivyo kwa sababu ya upungufu wa madarasa. Mhe. Jafo, alitoa miezi
miwili kwa serikali za mitaa kukamilisha ujenzi wa miundombinu hiyo. Je, fedha hizo
zilipelekwa? Na kama jibu ni ndiyo, je madarasa yaliyotegemewa yalijengwa? Na,
je wanafunzi walianza shule katika kipindi stahiki? Majibu haya yatawasaidia
wabunge na jamii kushauri ipasavyo.
amesema HakiElimu inatambua na inaipongeza serikali kwa
uamuzi wa kufuta kodi ya ongezeko la thamani (VAT) katika taulo za kike, uamuzi
uliofanyika katika bajeti ya mwaka 2018/19. Uamuzi huu ulichukuliwa kwa ajili
ya kutatua changamoto ya muda mrefu ya wanafunzi wa kike kushindwa kuhudhuria
shule kwa siku 2 hadi 3 kila mwezi kwa
sababu tu wanashindwa kukabiliana ipasavyo na namna ya kujihifadhi wakati wa
siku za hedhi kwa kutokuwa na uwezo wa kununua taulo za kike. Kuondoa kodi
kulitegemewa kungepunguza bei ya taulo za kike na kuzifanya ziweze kununuliwa
kiurahisi na watoto wanaotoka katika familia duni.
" Hata hivyo, utafiti mdogo
uliofanywa na HakiElimu katika soko la
bidhaa na kwa wanafunzi wa kike unaonesha kuwa kuna muitikio mdogo na sehemu
zingine hakuna utekelezwaji kabisa wa tamko hili la serikali. Katika maduka
mengi bei ya wastani ya taulo za kike ni ile ile ya shilingi 2,000/- ambayo
familia duni nyingi haziwezi kuimudu. Jambo hili linakatisha tamaa sana siyo tu
kwa wanafunzi wa kike bali hata kwa serikali."
amesema Waziri wa Afya, Maendeleo ya
Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Mhe. Ummy Mwalimu, aliwasilisha masikitiko yake
tarehe 15 Februari 2019 baada ya kugundua kuwa taulo za kike zinauzwa katika
bei ambazo walio na maisha duni hawawezi kuzimudu. Alisema kuwa ameandika barua
kwa Waziri wa Fedha na Waziri wa Viwanda na Biashara kuwasilisha masikitiko
yake. Ni matumaini yetu kuwa wizara itafuatilia suala hili. Pamoja na
hatua hii HakiElimu tunapendekeza serikali iangalie uwezekano wa
kufanikisha upatikanaji wa taulo za kike moja kwa moja mashuleni kama
ambavyo inafanyika kwenye baadhi ya nchi jirani.
alimaliza kwa kusema kuwa matumaini yao kuwa ushauri na maoni ya shirika hilo pamoja na wadau wengine utazingatiwa
ili kuinua ubora elimu nchini na hivyo kuchangia katika kufikia malengo ya Taifa ya kuwa na
uchumi wa kati ifikapo mwaka 2025.
Mmoja ya Wakurugenzi wasaidiz wa Shirika la Haki elimu nchini Godfrey Boniventure akifafanua jambo kwa Waandishi wa Habari juu ya Uchambuzi wa bajeti hiyo.
Sehemu ya Waandishi wa habari wakimsikiliza Mkurugenzi wa Shirika la Haki elimu Nchini,Dk John Kalage