MAJAMBAZI SUGU WANNE WAFARIKI DUNIA, JESHI LA POLISI LAKAMATA RISASI, BASTOLA, MILIPUKO YA KIENYEJI



Na mwandishi wetu, Globu ya jamii
JESHI la Polisi Kanda Maalum Dar es Salaam limewaua majambazi sugu wanne na kukamata silaha moja bastola aina ya Bereta iliyofutwa namba zake za usajili ikiwa na risasi moja ndani ya magazine na maganda manne ya risasi, tochi moja na milipuko miwili ya kutengeneza kienyeji.

Taarifa ya Kamanda wa Polisi Kanda maalum Dar es Slaam, SACP Lazaro Mambosasa imeeleza kuwa tarehe 15.08.2020 huko Kanga Nkinyerezi majira ya saa tisa na nusu alasiri kupitia kikosi kazi chake.

Katika tukio hilo awali alikamatwa mtuhumiwa aitwaye Nuru Thadei miaka 34, mkazi wa Kinyerezi kwa mahojiano ya matukio mbalimbali ya uhalifu, ndipo alikiri kuwa alikuwa gerezani kwa kesi ya mauaji ya Mchina maeneo ya kurasini mwaka 2011 kesi PI No.19/2011 na aliachiwa huru kutoka gerezani mwaka 2017 na kuunda genge la wahalifu na wenzake wengine walioachiwa gerezani.

Aidha jambazi huyo aliwaongoza askari kwenda kuwaonyesha walipo majambazi wengine na kuonyesha silaha wanazomiliki ndipo alipofika eneo la nyumba hiyo wanayoishi na kupanga mipango ya ujambazi alipiga kelele ndipo wale watuhumiwa wengine walianza kurusha risasi kuwaelekea askari, ndipo askari walijibu mapigo na kufanikiwa kuwajeruhi majambazi hao, Nuru Thadei na wenzake Godfrey Faustine, Antoni Mnyamongo na Peter Seba ambao walipofikishwa hospitali waligundulika kuwa wamefariki dunia. 

Taarifa hiyo inaeleza kuwa majambazi hao walikuwa na kesi za unyang’anyi wa kutumia silaha maeneo mbalimbali ya jiji.

Jeshi la Polisi likafanya upekuzi katika nyumba waliyokuwa wakiishi majambazi hao na kupata Pesa Tsh 600,000/=, simu za mkononi 5 aina mbalimbali, Laptop moja, Pete za ndoa, mabegi matatu na nguo ambazo ziliibiwa katika matukio ya uporaji ambazo zilihifadhiwa katika nyumba hiyo.

Sambamba na hilo wahanga wa matukio hayo walitambua mali zao zilizoibiwa na miili ya majambazi hao imehifadhiwa katika hospitali ya taifa Muhimbili kwa ajili ya utambuzi.

Post a Comment

Previous Post Next Post