Na Jane Edward, Arusha
Tanzania inatarajiwa kuwa mwenyeji wa mkutano wa 73 wa baraza la Kimataifa la viwanja vya ndege kanda ya Afrika ambapo dhamira ya mkutano huo ni kuendeleza maslahi ya pamoja ya viwanja vya ndege na kukuza ubora wakitaaluma ili kusaidia maendeleo endelevu sekta ya anga.
Akizungumza na waandishi wa habari Waziri wa Uchukuzi Profesa Makame Mbarawa amesema wizara yake kwa kushirikiana na Mamlaka ya viwanja vya ndege Tanzania(TAA)kuwa maandalizi ya mkutano huo unaendelea vizuri ambapo wajumbe wasiopungua 400 watahudhuria mkutano huo.
Amesema nchi wanachama 75 wa viwanja vya ndege wanaoendesha viwanja vya ndege zaidi ya 265 kati ya nchi 54 pamoja na washiriki 59 kwa pamoja watahudhuria mkutano huo ikiwemo kufanya mikutano ya bodi,kamati tendaji pamoja na kufanya maonyesho ya viwanja vya ndege mbalimbali.
Aidha kauli mbiu ya mkutano huo ni "katika kuelekea wakati ujao bora wa kijani kutumia usafiri wa anga endelevu na utalii wa ustawi wa kiuchumi".
Tukio hilo litaangazia maendeleo endelevu katika sekta ya usafiri wa anga na kuonyesha dhamira ya Tanzania katika utunzaji wa mazingira.
Abdul Mombokaleo ni Mkurugenzi wa Mamlaka ya viwanja vya ndege Tanzania(TAA) amesema menejiment imejipanga kuhakikisha inaimarisha matumizi ya Tehama katika viwanja vyote vya ndege pamoja na miradi ya kibiashara ili iweze kufanyika ikiwemo hati miliki ya viwanja hivyo kupatikana.
Amesema kuwa mkutano huo ni mkubwa na mamlaka ya viwanja vya ndege ni sekta mtambuka,kutokana na umuhimu huo mkutano unafanyika jijini Arusha na kwamba nchi itapata fursa ya kujitangaza ikiwemo vivutio vyake.
Amebainisha kuwa TAA wameendelea kuhakikisha masuala ya awali yanakamilika ikiwemo kumbi za mikutano na mchakato wa kumpata mgeni rasmi kwani wamejipanga vizuri kuhakikisha ugeni huo unakuwa salama katika siku zote utakaofanyika mkutano huo.
Mwisho...
.