Na Lusajo Mwakabuku, WANMM DODOMA
Uwezo mdogo kifedha kwa makampuni binafsi ya upangaji na upimaji yanayoendelea na kazi za urasimishaji nchini wa kuweza kumudu gharama za urasimishaji umetajwa kuwa moja ya sababu kuu zinazozorotesha kasi ya urasimishaji katika maeneo mbalimbali wanayofanyia kazi.
Hali hii imebainika baada ya kikao kilichofanyika jijini Dar es salaam kati ya wataalam kutoka Wizara ya Ardhi kwa kushirikiana na Ofisi za Ardhi Mikoa ya Dar es salaam na Pwani na Halmashauri zake walipokutana na wawakilishi/wamiliki wa makampuni yanayofanya kazi za urasimishaji katika mkoa wa Pwani kujadili changamoto zilizopo na kutafuta ufumbuzi wake ambapo asilimia kubwa ya makampuni haya yamemaliza muda wa mkataba kabla ya kazi kukamilika.
Akielezea lengo la kikao hicho, kiongozi wa kikosi kazi kilichoundwa na Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Bwana David Malisa alisema wizara imepokea malalamiko mengi kutoka kwa wananchi mbalimbali kuhusu kazi za urasimishaji. Kutokana na malalamiko hayo, wizara ikaunda timu ya kufanya tathmini na ufuatiliaji wa kazi zilizofanywa na kampuni za upangaji na upimaji kuhusu urasimishaji wa makazi yasiyopangwa nchini kwa kukutana na kampuni za upangaji na upimaji, mamlaka za upangaji, Kamati za urasimishaji na wananchi kwa lengo la kubaini changamoto zilizojitokeza katika zoezi la urasimishaji.
“Sisi tupo hapa kwa maelekezo ya wizara kuhakikisha kuwa tunapata ufumbuzi wa sababu zote zinazopelekea kukwama kwa zoezi la Urasimishaji. Kwa hiyo hatupo hapa kwa ajili ya kupata tathmini ya changamoto zilizopo peke yake, bali tupo hapa kuhakikisha kazi zinafanyika na malalamiko ya wananchi yanayotokana na kazi zenu nyie makampuni katika mitaa mbalimbali yanakwisha” Alisema Malisa.
Akiwakilisha kampuni ya Mataro Land Developers, Bwana Joel Mataro alisema wananchi wengi wamekuwa wana mwamko wa kushiki katika mazoezi ya urasimishaji ila shida inakuja wakati wa kulipia kile kiasi kilichopangwa ambapo kwa makampuni mengi kimekuwa ni shilingi 150,000 ambapo wananchi wamekuwa na mwamko mdogo na hivyo kusababisha kazi hii kuchelewa. Hoja hii ya mwamko mdogo wa kuchangia gharama iliungwa mkono makampuni mengine yaliyoshiriki kikao hiki.
Hoja hiyo ilipelekea kikosi kazi kuzitaka kampuni hizi kuhakikisha kazi inafanyika hasa kwa wale ambao tayari wamechangia bila kusubiri michango ya wananchi wote`. Aidha makampuni yameagizwa kutotegemea michango ya wananchi kama mtaji wa kufanyia kazi hizo na kazi zitoke kwa muda uliopangwa kwa mujibu wa mkataba. Aidha kikosi kazi kipo tayari kuhakikisha kinachangia huduma mbalimbali za urasimishaji ikiwemo uhamasishaji wa wananchi kutoa ushirikiano kwa makampuni katika kukamilisha kazi hizi.
Aidha changamoto nyingine iliyotajwa ni upitishwaji wa michoro ya mipango miji katika halmashauri ambapo wataalamu wakiletewa michoro na makampuni huifanyia kazi kwa wakati lakini michoro hiyo inapitia mlolongo mrefu ikiwa ni pamoja na kupitishwa na menejimenti ya halmashauri kabla ya kwenda wizarani. Hivyo ikaazimiwa kuwa kamishna wa ardhi mkoa amuandikie barua mkurugenzi ili aweze kuzipa kipaumbele kazi za urasimishaji.
Kikosi kazi hiki kimegawanywa katika timu tatu ambazo moja itafanya kazi katika mikoa ya Dar es salaam, Pwani na Morogoro, ya pili itakuwa Mkoani Arusha nay a tatu Dodoma.
Timu ya wataalam kutoka Wizara ya Ardhi, Ofisi za Ardhi Mikoa ya Dar es salaam na Pwani na Halmashauri wakiwa kikaoni na Makampuni yanayofanya urasimishaji Dar na Pwani kutatua changamoto za urasimishaji ardhi.
Kiongozi wa kikosi kazi kilichoundwa na Wizara ya Ardhi, nyumba na Maendeleo ya Makazi kukwamua kazi za urasimishaji katika Mikoa ya Dar es salaam, Pwani na Morogoro, David Malisa akisisitiza jambo katika kikao na makampuni yanayofanya kazi ya urasimishaji mikoani humo.
Baadhi ya wajumbe wa Halmashauri na ofisi ya Ardhi Mkoa wakifatilia majadiliano ya ukwamuaji kazi za urasimishaji ardhi katika maeneo yao.
Mwakilishi wa kampuni ya urasimishaji Perfect Land Planner & associates akielezea namna kampuni yake inavyopambana na changamoto za urasimishaji katika mitaa anayofanyia kazi mkoani Pwani.