NA MWANDISHI WETU
MKUU wa Wilaya ya Ileje, mkoani Songwe, Farida Mgomi, amesema kampeni ya msaada wa kisheria ya Mama ya Samia (Samia Legal Aid) imekuwa msingi mzuri wa kujenga uelewa kwa wananchi kuhusu haki zao za kikatiba na kisheria, jambo ambalo ni muhimu katika kulinda na kukuza haki za binadamu nchini.
DC Mgomi ametoa kauli hiyo mwishoni mwa wiki alipomwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Songwe, Godfrey Chongolo, kwenye uzinduzi wa kampeni ya Msaada wa Kisheria ya Mama Samia mkoani humo.
Amesema kampeni hiyo, imeonesha umuhimu wa pekee wa kuongeza wigo wa ufikiaji haki kwa wananchi hususani walio pembezoni.
Ameongeza kuwa, kauli mbiu ya Mama ya Msaada wa Kisheria ya Mama Samia inadhihirisha azma ya Rais Samia Suluhu Hassan ya kulinda, kukuza na kutetea haki za wanawake wanyonge na kupinga ukatili wa kijinsia, kulinda haki za binadamu na kuheshimu utawala wa sheria.
"Kupitia kampeni hii migogoro mingi ya kifamilia na kijamii iliyodumu kwa muda mrefu imesuluhishwa,ambapo hali hiyo imeleta utengamano katika familia na tija katika jamii.
"Nichukue fursa hii kuwasihi wananchi wa Songwe kuitumia vema fursa hii ambayo nasi tumebahatika kuipata,” amesema.
Amesema Wizara ya Sheria na Katiba imepewa dhamana ya kutekeleza majukumu ya Serikali yanayohusu masuala ya Katiba na Sheria za nchi, ambayo ni nyenzo muhimu katika kuhakikisha nchi yetu inaongozwa kwa misingi ya haki na utawala bora.
“Katika utekelezaji wa majukumu hayo, Wizara imeendelea kuzingatia miongozo mbalimbali ya kisera, kisheria, kikanuni na taratibu mbalimbali pamoja na maazimio ya kikanda na kimataifa ambayo nchi yetu imeridhia katika kusimamia masuala ya haki na utawala bora,”amesisitiza na kuongeza:
“Majukumu hayo yanatekelezwa kwa kuzingatia dhima ya Wizara ya Sheria na Katiba,ambayo ni kuwa na mfumo madhubuti ya sheria na kikatiba katika kufanikisha utekelezaji wa sera na mipango kwa maendeleo ya Taifa letu,” amesema.
Mwisho