MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu imeelezwa kuwa jumla ya mashahidi 15 na vielelezo tisa vinatarajiwa kuletwa mahakamani wakati wa usikilizwaji wa kesi ya uchochezi na kutoa taarifa za uongo inayomkabili Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo(Chadema), Tundu Lissu
Wakili wa Serikali Mkuu, Nasoro Katuga ameeleza hayo leo Mei 19, 2025 mbele ya Hakimu Mkazi Mwandamizi, Geofrey Mhini wakati kesi hiyo ilipoitwa kwa ajili ya mshtakiwa kusomewa maelezo ya awali (PH).
"Mheshimiwa idadi ya mashahidi tuliyoitaja ni iliyopo kwa sasa lakini kuna uwezekano tukapata mashahidi wengine hivyo tutaifahamisha mahakama iwapo kutakuwa na mabadiliko". Amesema Katuga.
Kesi hiyo imeahirishwa hadi Juni 2, 2025 kwa ajili ya kuanza kusikilizwa kwa mashahidi wa Upande wa Serikali huku Upande wa utetezi wakisema wao hawatataja sasa hivi idadi ya mashahidi walionao
Akisoma maelezo hayo ya awali Wakili wa Serikali Mwandamizi, Tawabu Issa alidai kuwa katika shtaka la kwanza Aprili 3, 2025 Dar es Salaam, kwa nia ya kudanganya Lissu alichapisha kupitia mtandao wa Youtube maneno yanayosema "uchaguzi wa serikali za mitaa 2024 wagombea wa CHADEMA walienguliwa kwa maelekezo ya Rais" wakati akijua sio kweli.
Tawabu alidai kuwa Aprili 3,2025 mkoani Dar es Salaam, Lissu kupitia mtandao wa Youtube alichapisha taarifa inayosema "Mapolisi wanatumika kuiba kura wakiwa na vibegi" wakati akijua sio kweli.
Vilevile katika shitaka la tatu Tawabu alidai kuwa Aprili 3,2025 mkoani Dar es Salaam akiwa na nia ya kudanganya umma, Lissu alichapisha katika mtandao wa Youtube maneno yanayosema "Majaji ni ma-CCM hawawezi kutenda haki wapate teuzi na kuchaguliwa kuwa majaji wa mahakama ya rufaa" wakati akijua tarifa hiyo ni uongo na inapotosha umma.
Lissu alikana mashtaka yote isipokuwa taarifa zake binafsi ambapo alidai kuwa maelezo yaliyotolewa si ya kweli lakini maneno yake aliyoyasema si ya uongo.
Aidha, Wakili wa utetezi aliiomba mahakama iamuru upande wa mashtaka wawapatie maelezo ya mtu aliyepeleka maelezo kusababisha kesi hiyo kufunguliwa ambapo Hakimu Mkazi Mwandamizi Mhini aliuagiza upande wa mashtaka kutekeleza ombi hilo.
Mwisho


