RC MTANDA AAGIZA MPANGO WA KUPUNGUZA MADENI YA WAZABUNI NA WATUMISHI MAGU




Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhe. Said Mtanda amesema Baraza la Madiwani linapaswa kufahamu madeni yote ya wazabuni na watumishi ili kuweka mpango wa kuyapunguza hatua kwa hatua katika miaka ijayo.

Mhe. Mtanda ametoa kauli hiyo leo Juni 25, 2026, alipokuwa akizungumza katika Mkutano Maalumu wa Baraza la Madiwani wa kujadili hoja za Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kwa Halmashauri ya Wilaya ya Magu.

Amesema ni muhimu kutambua wazabuni wanaodaiwa pamoja na kiasi wanachodai ili halmashauri iweze kuandaa mkakati wa malipo utakaosaidia kupunguza madeni hayo ndani ya kipindi cha miaka miwili hadi mitatu.

Aidha, ameeleza kuwa watumishi wanaoidai halmashauri wanapaswa kubainishwa pamoja na madai yao ili kuwepo mpango maalumu wa kulipa madeni hayo kwa awamu na hivyo kupunguza mzigo wa kifedha.

Mkuu huyo wa Mkoa pia amesisitiza kuwa fedha zote za Serikali zinazodaiwa lazima zirejeshwe, akizitaka halmashauri zote za Mkoa huo kuunda timu maalumu (task force) za kufuatilia na kukusanya madeni yote kuanzia mwaka 2023 hadi sasa.

Sambamba na hilo, amemshauri Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo kuimarisha ushirikiano na wataalamu wake bila ubaguzi, akisema hali ya mgawanyiko miongoni mwa watumishi huathiri utekelezaji wa majukumu na ufanisi wa kazi.

Kuhusu changamoto ya kutofautiana kwa majina ya baadhi ya watumishi, Mhe. Mtanda amesema atashirikiana na Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA) ili watumishi wenye tatizo hilo warekebishiwe taarifa zao na kuondoa hoja zilizotokana na changamoto hiyo.

Aidha, ameipongeza Halmashauri ya Wilaya ya Magu kwa kupata hati safi kwa miaka minne mfululizo, akibainisha kuwa imekuwa ikizalisha hoja chache za ukaguzi, huku nyingi zikiwa zimejibiwa na nyingine zikiendelea kufanyiwa kazi.



Post a Comment

Previous Post Next Post