MWENGE WA UHURU WAKABIDHI GARI LA WAGONJWA LUSHOTO

Na Ashrack Miraji, Lushoto

Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa, Bw. Wazo Mwang'onda, amekabidhi gari jipya la kubebea wagonjwa kwa Hospitali ya Wilaya ya Lushoto, akisema hatua hiyo ni sehemu ya juhudi za Serikali ya Awamu ya Sita za kuimarisha huduma za afya na kuwafikisha wananchi huduma muhimu kwa wakati.

Akizungumza wakati wa mapokezi ya Mwenge wa Uhuru yaliyofanyika katika viwanja vya Shule ya Msingi Kizala, wilayani Lushoto, Bw. Mwang'onda amesema ujio wa gari hilo unaonesha dhamira ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kuendelea kuboresha sekta ya afya kupitia ujenzi wa vituo vya afya, zahanati pamoja na upatikanaji wa magari ya wagonjwa katika maeneo mbalimbali nchini.

Kwa upande wake, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu – TAMISEMI na Mbunge wa Jimbo la Lushoto, Prof. Riziki Shemdoe, amemshukuru Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuwapatia wananchi wa Lushoto gari hilo, akieleza kuwa litasaidia kwa kiwango kikubwa kuboresha huduma za rufaa kwa wagonjwa wanaohitaji usafiri wa haraka kwenda kupata matibabu.

Prof. Shemdoe amesema gari lililokuwa likihudumia Hospitali ya Wilaya lilihamishiwa Kituo cha Afya Mlola ili kuimarisha utoaji wa huduma katika eneo hilo, hivyo ujio wa gari jipya unakwenda kuziba pengo lililokuwepo na kuongeza ufanisi wa huduma za afya katika wilaya hiyo.

Mkuu wa Wilaya ya Lushoto, Zephania Sumaye, amesema ujio wa gari hilo la kubebea wagonjwa unaakisi dhamira ya Serikali ya Awamu ya Sita ya kuendelea kuboresha huduma za afya kwa wananchi. Amesema uongozi wa wilaya utaendelea kusimamia matumizi sahihi ya gari hilo ili liweze kuwahudumia wananchi kwa ufanisi na kuongeza kasi ya utoaji wa huduma za dharura.

Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Lushoto, Dkt Ikupa Harrison amesema halmashauri itaendelea kuimarisha huduma za afya kwa kuboresha miundombinu, vifaa tiba na huduma za usafiri wa wagonjwa ili kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora na kwa wakati.

Katika hatua nyingine, Mwenge wa Uhuru umeendelea kutembelea na kukagua miradi mbalimbali ya maendeleo wilayani Lushoto, ikiwemo mradi wa barabara, hoteli ya kitalii, ukarabati wa matenki ya maji, ujenzi na ukamilishaji wa madarasa, mradi wa kuwawezesha vijana pamoja na Kituo cha Afya. Baada ya kumaliza shughuli zake wilayani humo, Mwenge wa Uhuru unatarajiwa kukabidhiwa Wilaya ya Korogwe kwa ajili ya kuendelea na mbio zake.







 

Post a Comment

Previous Post Next Post