WAZIRI MKUU MSTAAFU MIZENGO PINDA MGENI RASMI KONGAMANO LA KIMATAIFA LA WAFUGAJI WA NGURUWE BARANI AFRIKA






Na Lilian Ekonga Dar es Salaam, Septemba 3, 


Waziri Mkuu mstaafu wa Serikali ya Awamu ya Nne, Mhe. Mizengo Pinda, anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika kongamano kubwa la kimataifa la wafugaji wa nguruwe barani Afrika, linalotarajiwa kufanyika kuanzia Septemba 11 hadi 13, 2025, katika ukumbi wa Ubungo Plaza jijini Dar es Salaam.


Akizungumza na waandishi wa habari leo jijini Dar es Salaam, Mwenyekiti wa Chama cha Wafugaji wa Nguruwe Tanzania (TAFIPA), Bi. Dorine Maro, amesema  kongamano hilo ni la kwanza kufanyika nchini na linakusudia kuangazia mnyororo mzima wa thamani wa sekta ya ufugaji wa nguruwe.


“Ni tukio la kihistoria kwa Tanzania. Hatujawahi kuwa na kongamano la aina hii linalozihusisha nchi mbalimbali za Afrika kwenye sekta ya ufugaji wa nguruwe,” amesema Dorine.


Bi. Dorine alieleza kuwa kongamano hilo litawakutanisha wadau mbalimbali waliopo kwenye mnyororo wa thamani wa ufugaji wa nguruwe, wakiwemo wataalamu, watafiti, taasisi za fedha na sekta binafsi. Wafugaji watajifunza kuhusu teknolojia mpya, tafiti za kisayansi na fursa za kiuchumi zilizopo kwenye sekta hiyo.


Zaidi ya vyama tisa vya wafugaji kutoka nchi mbalimbali barani Afrika tayari vimethibitisha kushiriki, huku akihimiza washiriki binafsi na makampuni kujisajili mapema ili waweze kushiriki kikamilifu. Alitoa wito kwa makampuni yanayopenda kudhamini kongamano hilo kujitokeza kuunga mkono juhudi hizo.


Kuhusu hali ya ulaji wa nyama ya nguruwe nchini, Dorine alisema kuna ongezeko kubwa la mahitaji, jambo linaloonesha ukuaji wa soko. Hata hivyo, aliitaka serikali kuangalia changamoto zinazoikabili sekta hiyo, hususan miundombinu duni ya machinjio ya kisasa.


Kwa upande wake, Meneja Masoko wa Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB), Bw. Richard Stiveni – ambaye ni mdhamini wa kongamano hilo – aliwahamasisha wafugaji kujitokeza kwa wingi ili kunufaika na elimu ya fedha na fursa za mikopo zinazotolewa na benki hiyo.


“Kupitia kongamano hili, wafugaji watapata maarifa yatakayowasaidia kukuza biashara zao kwa kutumia huduma za kifedha zinazotolewa na TADB,” amesema  Bw. Stiveni.


Kongamano hilo linatarajiwa kuwa chachu ya maendeleo ya sekta ya ufugaji wa nguruwe nchini na Afrika kwa ujumla, kwa kuimarisha ushirikiano, kuongeza thamani ya bidhaa na kuboresha maisha ya wafugaji.











Post a Comment

Previous Post Next Post