Mwekezaji mmoja mwenye asili ya Kisomali ameibua sintofahamu katika Halmashauri ya Manispaa ya Temeke baada ya kujenga katika bonde la hifadhi ya Mto Kizinga kinyume na taratibu za kisheria, hali iliyowahusisha viongozi wa halmashauri, Mkuu wa Wilaya pamoja na Baraza la Madiwani.
Mwekezaji huyo, anayejenga katika eneo la hifadhi ya mto na barabara, ametajwa na Mkuu wa Wilaya ya Temeke, Sixtus Mapunda, pamoja na Diwani wa Kata ya Kijichi, kuwa amefanya ujenzi huo bila kufuata taratibu na miongozo ya mipango miji.
Akizungumza wakati wa ufunguzi wa kikao cha Baraza la Madiwani, DC Mapunda alisema ni jambo la kushangaza kuona mtu anajenga katika eneo la hifadhi ya Mto Kizinga na hifadhi ya barabara kisha anapatiwa vibali vya ujenzi pamoja na hati miliki kutoka wizara husika.
“Ni jambo la ajabu mtu anajenga kwenye hifadhi ya mto na barabara halafu anapewa hati. Ameenda mbali zaidi hadi kuingilia maeneo ya wananchi waliokwisha fidiawa na Serikali zaidi ya miaka 20 iliyopita,” alisema Mapunda.
Aidha, DC Mapunda aliipongeza Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) kwa kusimamia sheria, akisema hadi sasa hawajatoa kibali chochote cha mazingira kwa eneo hilo.
Kwa upande wake, Diwani wa Kata ya Kijichi, Mhe. Tibelyo Exavery Kalinga, alihoji hatua zilizochukuliwa na Halmashauri ya Manispaa ya Temeke dhidi ya mwekezaji huyo anayejenga kwenye hifadhi ya mto na barabara.
Akijibu swali hilo, Mkurugenzi wa Manispaa ya Temeke, Joumary Satura, alisema hana taarifa rasmi za kiutawala kuhusu ujenzi huo, na kuahidi kuwa atatembelea eneo husika akiwa na wataalamu kwa ajili ya tathmini na hatua stahiki.
Suala hilo linaendelea kufuatiliwa huku viongozi wakisisitiza kuwa hakuna mtu aliye juu ya sheria, hasa linapokuja suala la ulinzi wa hifadhi za mazingira na miundombinu ya umma.


