Kamati ya Kupinga Ukatili wa Wanawake na Watoto (MTAKUWWA) Wilayani Magu imetakiwa kuongeza juhudi za kutoa elimu kwa jamii ili kutokomeza vitendo vya ukatili wa kijinsia vinavyoendelea kushamiri wilayani humo.
Rai hiyo imetolewa leo Julai 1, 2026 na Mwenyekiti Mwenza wa Kamati ya MTAKUWWA Mkoa wa Mwanza, Yassin Ally, wakati wa kikao na Kamati ya MTAKUWWA Wilaya ya Magu kilichofanyika katika ukumbi wa Halmashauri ya Wilaya ya Magu. Amesema vitendo vya ukatili vimeendelea kuwa kikwazo kwa maendeleo ya wananchi na vinahitaji ushirikiano wa wadau wote kuvimaliza.
Amesema bado kuna changamoto katika sekta ya elimu, akieleza kuwa baadhi ya walimu hukimbia vituo vyao vya kazi kutokana na vitisho na matukio ya ushirikina, hali inayosababisha taharuki na kuathiri utoaji wa huduma za elimu.
Aidha, ameeleza kuwa baadhi ya wazazi huwapa watoto wa kike mafundisho potofu ya kujifelisha kwa makusudi katika mitihani ya kuhitimu ili waolewe mapema, akisisitiza kuwa tabia hiyo inapaswa kukemewa.
Kwa upande wake, Afisa Ustawi wa Jamii Mkoa wa Mwanza, Baraka Makona, amesema Kamati ya MTAKUWWA Mkoa inaendelea na ziara katika wilaya zote za mkoa huo kwa lengo la kufuatilia utekelezaji wa mipango ya kupambana na ukatili wa kijinsia pamoja na kubaini changamoto zinazojitokeza.
Awali, Afisa Ustawi wa Jamii Wilaya ya Magu, Coletha Sanga, amesema kupitia jitihada za kuwawezesha wananchi kiuchumi, Halmashauri imetoa mikopo yenye thamani ya zaidi ya shilingi milioni 330 kwa vikundi 28 ili kusaidia kupunguza umasikini na kuongeza ustawi wa jamii.






