JUKWAA LA KATIBA KWENDA MAHAKAMANI KUDAI MAANDAMANO

 JUKWAA la Katiba Tanzania (Jukata), limesema kuwa litalifikisha jeshi la Polisi Mahakamani, kudai haki ya kikatiba kufuatia kuzuiwa kufanya maandamano ya amani.

Shauri hilo litaongozwa na jopo la mawakili wakiongozwa na Dk. Rugemeleza Nshala kudai haki hiyo. 

Mwenyekiti wa Jukata Hebron Mwakagenda alisema jana jijini Dar es Salaam, kuwa hatua hiyo imekuja kufuatia Jeshi la Polisi Kanda Maalum Dar es Salaam kuzuia maandamano yaliyotakiwa kufanyika Oktoba 30mwaka huu.

Alisema barua kutoka jeshi hilo ikielezea kwamba maandamano hayo yataathiri mitihani ya Kidato cha nne inayoendelea nchini, kutojibiwa barua na Ikulu ya kukubaliwa ili rais apokee maandamano hayo, ni sababu ambazo hazina msingi.

"Hadi Leo hatujapata majibu ya barua iliyotumwa Ikulu kwa Rais, juu la ombi ingawa lakini jeshi limetuandikia barua kutuzuia, kabla ya kukataliwa au kukubaliwa na Rais," alisema Mwakagenda.

Alisema Jukata lilipanga kufanya maandamano hayo ili kuunga mkono jitihada ya Rais John Magufuli katika kusimamia rasilimali za taifa, kupiga vita rushwa pamoja na kukumkumbusha kuendeleza mchakato wa Katiba mpya.

Pia maandamano yalilenga kufikisha ujumbe wa wananchi kwa rais kuhusu haja ya serikali kurejesha mchakato huo, ili ipatikane katika uongozi wa awamu ya tano.

Mwakagenda alisema wanatatajia mahakamani itaeleza kwa namba gani wananchi wanapaswa kutumia haki ya kikatiba.

"Ibara ya 107 (A) (1) inasema ..Mahakama ndio yenye kauli ya mwisho ya utoaji haki katika Jamhuri ya Muungano itakuwa ni Mahakamani," alisema.

Alisema mahakama pia itatoa tafsiri ya mahakama kuhusu namna jeshi la polisi linavyotumia vifungu 43 (3) na 44 vya sheria ya jeshi la polisi ya mwaka 2002.

"Taarifa za kiintelijensia kwamba kuna viashiria vya uvunjifu amani havina ukweli, mahakama itatuamulia," alisema Mwakagenda.

Post a Comment

Previous Post Next Post