Meneja Hafidh karibu tena



ABDULAH MKEYENGE

-NIMEWAHI kukutana na watu wakarimu, wanyenyekevu, waungwana katika soka letu, lakini Hafidh Saleh ni namba moja katika watu wote hao. Jamaa ni bonge la mshikaji.

- Leo tumzumgumzie kidogo Hafidh. Jamaa amerudishwa tena Yanga katika nafasi ya Umeneja wa timu. Hii ni nafasi inayomtosha kabisa. Sio kubwa, wala ndogo. Ni size yake.

- Hafidh alikuwa sehemu ya watu waliondolewa kazini kipindi kile pamoja na kina Mwinyi Zahera. Alibaki kuwa mkimya na kusimama nyuma ya timu kadri alivyoweza.

- Hakununa wala hakusengenya alipoondolewa kazini. Ni tofauti na watu wengi wakiondolewa kazini Simba, Yanga.

- Hafidh alibaki kuiunga mkono timu licha ya kutokuwa sehemu ya timu. Mechi nyingi za Yanga alikaa jukwaani. Alifurahia Yanga iliposhinda, aliumia Yanga ilipopoteza. Ni mtu tofauti. Watu wengi wakiondolewa huomba mambo mabaya yatokee. Hafidh sio wa hivi.

-Binafsi niliendelea kumuita Meneja. Nilimuita hivi na aliniitikia. Hakuwahi kuniambia nisimuite jina hilo ambalo kwa wakati huo hakuwa analo.

-Uzoefu wake kazini, sijui kama 🇹🇿 tuna Meneja wa viwango vyake katika nyakati hizi. Ana uzoefu wa kutosha na kazi hii. Kama ameifanya kwa miaka michache inafika miaka 7, lakini yuko muda mrefu katika nafasi hiyo na anayajua majukumu yake.

-Ni Hafidh anayejua timu ikifika nchi kama Misri ikakae hoteli gani na ifanye mazoezi katika uwanja upi. Ni Hafidh huyo huyo anayejua timu ikifika Angola ikae hoteli gani na ifanye mazoezi katika kiwanja kipi.

 -Sijui kama nchi ina Meneja wa kiwango hiki kando ya Hafidh. Sijui! Yanga mpya chini ya Senzo imefanya jambo jema kumrudisha kazini Hafidh. Ni huyu anayekwenda kuirudisha timu katika mstari. 

-Tuna Mameneja wengi wenye mahusiano duni na Waandishi, lakini Hafidh ni rafiki wa waandishi wengi. Sidhani kama kuna Mwandishi mwenye uhusiano duni na Hafidh.

- Mpigie simu kutaka taarifa anakupa ushirikiano. Kama jambo haliko ndani ya uwezo wake anakwambia. Ikiwezekana anakuunganisha na mtu wa kumfuata upate msaada. Kuna Mameneja, kisha kuna Hafidh.

-Meneja wa Simba rafiki yangu Patrick Rweyumamu ni mtu mwingine Muungwana mwenye mengi ya kujifunza kwa Hafidh. 

Karibu tena Meneja Hafidh.

Post a Comment

Previous Post Next Post