ABDULAH MKEYENGE
- KWA mara nyingine tena Hassan Mwakinyo ameshinda pambano lake na kusema anawashukuru Watanga wenzake, baadae akasema anawashukuru na Watanzania.
- Inawezekana akawa anawapenda sana Watanga wenzake, lakini kwa level aliyoko sasa Mwakinyo anapaswa kuitaja Tanzania mara nyingi zaidi na sio Utanga wake.
- Siku nyingine tena katika pambano lake dhidi ya Mkongomani, Mwakinyo alisema anashukuru kuona Watanga wenzake waliopoteza usingizi ili kumtazama. Vipi kwa Watanzania wengine waliopoteza usingizi wao kumtazama, lakini sio watu wa Tanga?
- Diamond Platinum anajisifia Utanzania wake. Mbwana Samatta anajisifia na Utanzania wake, vipi Mwakinyo anayejisifu na Utanga wake? Tanzania ndiyo baba yetu. Tanzania ndiyo mama yetu. Ni vyema aanze kujifunza kuitamka mara nyingi zaidi.
- Mwakinyo alivyomaliza pambano lake na Mphilipino nilisikiliza maoni yake na shukrani. Aliitaja Tanga katika sehemu nyingi na Tanzania sehemu chache. Nilimuuliza moja ya watu wa Tanga Hafidh Kido kuhusu Mwakinyo na tabia hii.
- Sikumbuki Kido alinipa jibu gani juu ya swali lile, lakini jana Mwakinyo amerudia kile kile alichokifanya dhidi ya Mphilipino. Ni vyema watu wa timu yake wanaomzunguka kumjenga katika Utanzania zaidi, sio Utanga zaidi.
- Nafahamu ni fahari kupataja kwenu mbele ya watu wengine. Ina raha yake, lakini ukishafika hadhi kama ya Mwakinyo huwi tena bondia wa Tanga, unakuwa bondia wa Tanzania. Mwakinyo alifanyie kazi hili.
-Katika kilele cha ubora wa Rashid Matumla sikumbuki kama aliwahi kuitaja Keko au Dar es Salaam. Aliitaja zaidi Tanzania. Kama Mwakinyo akicheza dhidi ya Mtanzania mwenzake anaweza kuitaja Tanga, lakini mechi za kimataifa anapaswa kuitaja nchi.
- Mwakinyo ndiye aliyebeba bendera ya nchi katika masumbwi hivi sasa. Kama nchi tunajulikana kwa masumbwi kupitia yeye, hivyo lazima aishi kama Mtanzania, sio Mtanga.
-Watanzania wenzake mara nyingi wamesimama nyuma yake katika nyakati zote ngumu na nyepesi anazopitia. Hivyo anaposimama mbele ya hadhara na kuitaja Tanga, anamvuluga Mtanzania aliyeko Sengerema au Kilwa.