WAZIRI wa Ardhi,Nyumba na Maendeleo ya Makazi,Deogratius Ndejembi ametoa maelekezo kwa Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) kuhakikisha wanafata malengo ya shirika ya mwaka 1962,yaliyowekwa na Baba wa Taifa Hayati Julius Nyerere ya kuhakikisha wanawajengea watanzania nyumba zilizobora na zenye bei nafuu.
Akizungumza jana jijini Dar es Salaam,wakati alipotembelea Shirika hilo kwa lengo la kujitambulisha kwa menejimenti ya shirika hilo,Ndejembi alisema shirika la NHC linaenda vizuri na kuingiza faida ipasavyo.
Alisema katika kufanya majukumu yao NHC wanapaswa kutowasahau na kutowaacha nyuma watanzania kwa kuhakikisha wanakuwa na mipango mizuri ya kuhakikisha watanzania wanamiliki nyumba.
"Tunapaswa kuhakikisha mtanzania anayejenga nyumba yake taratibu kwa fedha anazofanya kazi au mjasiliamali aliyejipatia fedha zake ,tuhakikishe tunamrahisishie ndoto yake ya kupata nyumba kwa bei nafuu na iliyobora," alisema na kuongeza.
"Tunapaswa kutokusahau malengo na maono ya Baba wa taifa Julius Kambarage ya kuhakikisha watanzania wanapata nyumba bora kama vile maono yake yalivyokuwa yanataka,"alisema.
Alisema nyumba zinazojengwa zinapaswa kuwa za bei nafuu kwa watu wote, kuwa za viwango bora na ziwe katika maeneo yanayofikika kwa urahisi na isiwe kilometa 100 mbali na maeneo ya shughuli zao.
Waziri Ndejembi alisema mbali na hiyo shirika hilo linatakiwa kuhakikisha miradi wanayofanya inaonyesha thamani ya fedha.
"Hakikisheni miradi yetu kuwa na value of money ,niwaombe umakini katika miradi katika hatua kwa hatua hususan katika manunuzi ya maeneo kwenye mauzo na kuhakikisha hakuna wizi,"alisema.
Aidha aliwapongeza kuwepo kwa mradi wa Samia Housing Scheme,kuwa na lengo la kujenga nyumba 5000, jambo hilo ni zuri hivyo ni jukumu la kuangalia maeneo ambayo yanauwezo wa kuwapata watu wengi zai ambao hawajafikia.
"Tusiache malengo yetu 1962 kuhakikisha tunajenga nyumba za kiwango kwa watanzania hasa kwa wale wa kipato cha chini,tuchanganye kwa jengo moja tunauza na nyingine tunapangisha kwa kipato cha chini nyumba ambazo ni za bei nafuu.
"Tukumbuke tunatengeneza mfumo ambao mtu atakuwa anauwezo wa kulipa asilimia 10 au 20 ya nyumba alafu anaingia kwenye nyumba alafu anakuwa analipa kodi kama kawaida ,baada ya hapo malipo haya yanayolipwa yanaingia katika ununuzi wake ambapo baada ya miaka 5 au 10 nyumba inakuwa yake,"alisema .
Awali alipokuwa anawasilisha taarifa fupi Waziri huyo kuhusu shirika lao ,Mkurugenzi wa NHC ,Hamad Abdallah alisema miongoni mwa jukumu lao kama NHC ni pamoja na kujenga nyumba za makazi na majengo mengine kwaajili ya kuuza na kupangisha.
Alisema shirika linajumla ya majengo 2872 yenye sehemu ya kupangisha zipatazo 20,349 ambapo rasilimali hizo zinaleta shirika kuwa na mtaji w Trilion 5.6.