Watatu Kizimbani Kwa Biashara Ya Zaidi Ya Kilogramu 53.93 za Dawa Za Kulevya.

 

Na Mwandishi Wetu


MFANYABIASHARA Geofrey Barnabas (29) na wenzake wawili wamefikishwa katika mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kujibu tuhuma za kujihusisha na dawa za kulevya na kufanya biashara ya dawa za kulevya mauna ya Codeine zenye uzito wa jumla ya Kilogramu  53.93


Katika hati ya Mashtaka iliyosomwa mahakamani hapo na wakili wa serikali Tumaini Mafuru imewataja washtakiwa wengine kuwa ni, wafanyabiashara Issaya Japhet (30) na Jovistus Butatondewe (27) wote wakazi wa Mongo la Ndege Ukonga.


Mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu Gwantwa Mwankuga inadaiwa Oktoba 9, 2024 katika ofisi za DHL zilizopo Uwanja wa ndege wa Mwalimu Nyerere alikutwa akifanya biashara ya dawa za kulevya aina ya Codeine zenye uzito wa kilogramu 14.52


Katika shtaka la pili inadaiwa siku hiyo hiyo huko Ukonga eneo la Mongolandege wilaya ya Ilala mkoa wa Dar es Salaam washtakiwa wote watatu kwa pamoja walikutwa wakifanya biashara ya dawa ya kulevya aina ya Codeine kilogramu zenye uzito wa kilogramu 39.41.


Hata hivyo washtakiwa hawakuruhusiwa kujibu kitu chochote mahakamani hapo kwa kuwa mahakama hiyo haina mamlaka ya kusikiliza kesi ya uhujumu uchumi. 


Wakili Mafuru amedai upelelezi wa kesi hiyo bado haujakamilika na kesi hiyo imeahirishwa hadi Disemba17,mwaka huu kwa ajili ya kutajwa.



MWISHO.

Post a Comment

Previous Post Next Post