Na Hamis Shimye
KUANZA kazi ya kusafirisha abiria kwa Meli ya New Victoria Hapa Kazi Tu, baada ya kusitisha kwa shughuli zake kwa zaidi ya miaka sita ni heshima kubwa aliyotupa Watanzania, Rais Dk. John Magufuli na serikali nzima kwa ujumla.
Hii ni historia kubwa kwa wakazi wa kanda ya ziwa, ambao walikuwa wanateseka hasa kutokana na kukosekana kwa usafiri huo ambao utakuwa unakwenda kuamsha uchumi kwenye maeneo mbalimbali ikiwemo Jiji la Mwanza na Bandari za Kemondo Bay na Bukoba mkoani Kagera.
Kukamilika kwa ukarabati huo uliofanywa na serikali kwa zaidi ya sh. bilioni 22.4 ni historia kwa kuwa serikali imeamua kutatua shida kubwa ya wananchi kukosa usafiri wa uhakika kwa wakazi wa Kanda ya Ziwa.
Uwepo wa meli hiyo kongwe iliyojengwa mwaka 1960 ni ukombozi mkubwa na Rais Dk. Magufuli anastahili heshima kwa kuwa amekuwa kiongozi anayezungumza na kutenda hasa kutokana na kutekeleza ahadi yake ya ukarabati wa meli hiyo kwa haraka na kwa wakati.
Japokuwa uzinduzi rasmi wa meli hizo bado na kilichofanyika sasa ni kuanza kwa safari kwa meli hiyo pamoja na meli ya New Butiama, lakini hili linapaswa kupongezwa kwa kiasi kikubwa na kila mpenda maendeleo kwa kuwa limekuja wakati mwafaka wa kila mtanzania kushuhudia maendeleo.
Maendeleo yaliopo sasa na yanayoendelea kuletwa ni sehemu ya kila mpenda maendeleo kusema AHSANTE RAIS DK. MAGUFULI kwa kuwa bila usimamizi madhubuti kutoka kwa yeye binafsi, meli hiyo isingejengwa na hata kufufua usafiri wa meli katika Ziwa Victoria.
Kwa miaka mingi kulikuwa na shida kubwa ya usafiri kwa abiria na wafanyabiashara na hata kusababisha kukosekana kwa fedha nyingi ambazo taifa zingepatikana kutokana na usafirishaji wa mizigo na abiria ungekuwepo.
Sasa kuna usafiri wa uhakika kwa wakazi wa Mwanza na Nansio, Ukerewe hasa kutokana na uwepo wa meli bora na imara ya New Butiama huku pia kwa wakazi wa Kagera nao sasa wanausafiri wa uhakika baada ya kuukosa kwa muda mrefu kutokana na kutokuwepo kwa meli.
Kuanza kazi kwa meli hizo sasa ni wakati wa kuchangamsha uchumi wa nchi hasa wa Kanda ya Ziwa na maeneo yote, ambapo sasa bandari zilizopo Kanda ya Ziwa, zitaanza kufanya kazi kwa kasi kubwa kutokana na uboreshaji wa meli hizo.
Pia, huu ni wakati wa Kampuni ya Huduma za Meli (MSCL) Ltd, kuhakikisha inajipanga vyema katika biashara ya usafirishaji, ambao ni bora na salama. Hii inatokana na heshima kubwa anayoendelea kutupa Rais Dk. Magufuli ambaye anazidi kuandika historia kuanzia angani na sasa tuko majini.