________
Watu wengi wameniuliza sana kuhusu kongamano la viongozi wa DINI. Siwezi kumjibu kila mtu peke yake. Maoni yangu ni haya:
1. Hakuna DINI inayoiwakilisha nyingine. Wasikilizeni walioenda. Msiwapuuze ambao hawakwenda maana nao wana DINI zao. Ndio maana COVID 19 imeshindwa Tanzania kwa sababu ya MAOMBI ambayo wengine (waliokuwa Ulaya) wanabeza.
2. Nyakati za uchaguzi huwa kuna kutumiana. DINI kuitumia serikali au serikali kuitumia DINI katika kufanya maombi ili chaguzi zipite kwa amani na utulivu. Mungu yuko pande zote na hatumwi wala hatumiwi bali ANATUMA ili Malaika zake watende sawasawa na mapenzi yake.
3. Taifa linaunganishwa na kamati za AMANI na HAKI. Waandaaji wa kongamano wamesema hili ni Kongamano la AMANI na HAKI. Wanaotaka shari, wasubiri kongamani jingine.
4. Uchaguzi maana yake ni kuchukua kimoja kilicho bora kati ya vingine visivyo bora. Tusichukiane kwa mtu kuutumia Uhuru wake kuchagua anachopenda. Kila mtu aheshimu uchaguzi wa mwenzake. Tuache kuhukumu wengine kwamba wanachanganya DINI na SIASA. Kongamano hili halijachanganya DINI na maharage bali kuna uwepo wa Mungu, mpenda AMANI na HAKI.
5. DINI si mali za viongozi tu katika jamii na si mali ya Vyama vya kisiasa. Si mali pia mali ya viongozi wa DINI. Lakini vyote (DINI, vyama na serikali) havimmiliki Mungu bali Mungu anavimiliki. Hata hivyo Kongamano limemtanguliza Mungu. Inapendeza, lakini wakumbuke:
-Mungu halindwi, analinda
-Mungu habebwi, anabeba
-Mungu haamrishwi, anaamrisha
-Mungu hamilikiwi, anamiliki
-Mungu si tukio ni mchakato.
Haya ni maoni yangu, nawe una yako. Uwe na AMANI katika Mambo yako Kama nilivyo na AMANI na Mambo yangu.!
Mpende Kiongozi wako aliye BORA. Mpende Mzalendo; Mpende anayejali wengine; Mpende Mcha Mungu. Wapende Watanzania na usimpende anayetumiwa na WASIOITAKIA NCHI YETU MEMA.